Bunge la Taifa limepiga kura na kupitisha hoja maalum ya kumuondoa madarakani Naibu Rais Rigathi Gachagua.
Hii ni baada ya wabunge 281 kuunga mkono hoja hiyo iliyowasilishwa na mbunge wa Kibwezi Magharibi Mwengi Mutuse.
Mutuse aliwasilisha mashtaka 11 dhidi ya Gachagua kwenye hoja yake ikiwa ni pamoja na kueneza semi za chuki na kujilimbikizia mali kwa njia ya kutilia shaka.
Wabunge 44 walipiga kura ya kupinga hoja hiyo iliyozua mjadala mkali bungeni huku Gachagua akiwa kitovu cha shutuma za wabunge wengi.
Ni mbunge mmoja aliyejizuia kupiga kura huku baadhi ya wabunge ambao awali walikuwa wametia saini hoja hiyo wakiamua kutohudhuria kikao hicho.
Jumla ya wabunge 291 walikuwa wametia saini hoja hiyo.
Awali, Naibu Rais alifika katika bunge hilo na kujitetea dhidi ya madai aliyolimbikiziwa.
Kufuatia kupitishwa kwa hoja ya kumtimua Gachagua madarakani, Spika wa Bunge la Taifa Moses Wetang’ula sasa atahitajika kumtaarifu Spika wa Bunge la Seneti Amason Kingi kuhusiana na uamuzi wa Bunge la Taifa.
Hii ni kwa mujibu wa kifungu 145 (b) cha katiba.
Kisha Kingi anatarajiwa kuitisha kikao cha Maseneta kuangazia uamuzi wa Bunge la Taifa, na ama kukubaliana nao au kuukatalia mbali.
Ikiwa Seneti itakubaliana nao, basi Gachagua atavuliwa wadhifa wa Naibu Rais.
Hata hivyo, katika hali kama hiyo, Gachagua anaweza kuelekea mahakamani na kupata agizo la kuzuia kuondolewa kwake madarakani.
Katika hali kama hiyo, itabidi aendelea kuhudumu kwenye wadhifa huo hadi kesi aliyowasilisha mahakamani kupinga kuondolewa kwake madarakani isikizwe na kuamuliwa.
Timu ya Gachagua inatazamia kuwa mchakato wa kusikiliza kesi hiyo, kuanzia Mahakama Kuu hadi kwenye Mahakama ya Upeo ikiwemo ukataji rufaa, utakuchukua muda unaoweza kuhakikisha Gachagua anaendelea kuhudumu hadi muhula wa sasa ukamilike.