Bunge la Taifa kurejelea vikao vyake leo Jumanne

Martin Mwanje
2 Min Read
Vikao vya bunge

Bunge la Taifa litarejelea vikao vyake leo Jumanne baada ya kuwa kwenye mapumziko mafupi ya wiki tatu zilizopita.

Itakuwa mara ya kwanza kwa bunge hilo kurejelea vikao hivyo tangu lilipovamiwa Juni 25 mwaka huu na waandamanaji waliolalamikia kupitishwa kwa Mswada wa Fedha 2024.

Kwenye ajenda yake ya kwanza linaporejea, bunge hilo linatazamiwa kuanza mchakato wa kupigia msasa orodha ya kwanza ya mawaziri 11 walioteuliwa na Rais William Ruto kuhudumu katika Baraza Jipya la Mawaziri.

Orodha nyingine ya mawaziri inatarajiwa kutangazwa yamkini wiki hii.

Spika wa bunge hilo Moses Wetang’ula ametangaza kuwa mawaziri wote walioteuliwa watapigiwa msasa, licha ya kwamba baadhi yao walihudumu katika Baraza la Mawaziri lililovunjwa na Rais Ruto.

Mawaziri hao ni Prof. Kithure Kindiki aliyeteuliwa kuhudumu kama Waziri wa Usalama wa Kitaifa, Aden Duale (Ulinzi), Davis Chirchir (Barabara na Uchukuzi), Soipan Tuya (Mazingira) na Alice Wahome (Ardhi).

Waziri wa zamani wa Biashara Rebecca Miano ameteuliwa kuwa Mwanasheria Mkuu.

Mawaziri wapya ambao pia wanatarajiwa kupigiwa msasa ni Dkt. Debra Mlongo Barasa (Afya), Julius Ogamba (Elimu), Dkt. Andrew Karanja (Kilimo), Eric Muriithi (Maji) na Dkt. Margaret Ndung’u (Habari, Mawasiliano na Uchumi wa Dijitali).

Wabunge hao wanarejelea vikao vyao wakati ambapo vijana wa Gen Z wametangaza kuwa watafanya maandamano leo Jumanne, hatua ambayo huenda ikaibuoa kumbukumbu ya hofu iliyowazonga vijana hao walipovamia bunge muda mfupi kabla ya kwenda mapumzikoni.

Majengo ya bunge ni miongoni mwa maeneo ambayo usalama umeimarishwa mno kabla ya kufanyika kwa maandamano ya hii leo.

Share This Article
Leave a Comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *