Bunge la Seneti kujadili mswada kuhusu tabia nchi kwenye kikao maalumu

Marion Bosire
1 Min Read

Spika wa bunge la Seneti Amason Kingi ametangaza kikao maalumu cha bunge hilo Alhamisi Agosti 31, 2023 kupitia gazeti rasmi la serikali. Kwenye kikao hicho, maseneta watajadili mswada wa marekebisho ya sheria kuhusu mabadiliko ya tabia nchi.

Mjadala na maamuzi kuhusu mswada huo vinastahili kukamilika kabla ya Kongamano la Afrika kuhusu Tabia Nchi litakaloandaliwa jijini Nairobi Septemba 4 hadi 6.

Spika Kingi alisema maseneta siku hiyo, watajadili pia mabadiliko kwenye kalenda ya bunge hilo ili kuruhusu kuandaliwa kwa kikao cha pili.

Kwenye arifa hiyo, Kingi alisema kwamba mada aliyotaja ndiyo pekee itajadiliwa kwenye kikao hicho na baada ya hapo, vikao vya bunge vitaahirishwa hadi Septemba 5, 2023, kulingana na kalenda ya bunge hilo.

Maseneta kwa sasa wako kwenye likizo na hili linajiri siku moja tu baada yao kuandaa kikao maalumu cha kuidhinisha kamati ya mazungumzo ya kitaifa.

Kongamano la Afrika kuhusu Tabia Nchi lialenga kuharakisha utekelezaji wa sera za kusuluhisha tatizo la mabadiliko ya tabia nchi.

Share This Article