Bunge la Seneti limeidhinisha hoja ya kumuondoa mamlakani Naibu Gavana wa kaunti ya Kisii Dkt. Robert Monda.
Dkt. Monda anakuwa Naibu Gavana wa kwanza kutimuliwa madarakani tangu kufanyika kwa uchaguzi mkuu wa mwaka 2022.
Kadhalika, yeye ndiye Naibu Gavana wa kwanza kuondolewa mamlakani tangu kuanza kutekelezwa kwa mfumo wa ugatuzi mwaka wa 2013 chini ya katiba mpya ya mwaka 2010.
Dkt. Monda alikabiliwa na mashtaka manne yaliyojumuisha ukiukaji wa katiba, utumizi mbaya wa mamlaka, ukiukaji wa sheria na uhalifu.
Wakati wa kikao cha bunge la Seneti jana Alhamisi, Dkt. Monda alipatikana na hatia ambapo maseneta 39 walipiga kura kuunga mkono mashtaka ya kukiuka katiba, 35 waliunga mkono mashtaka ya matumizi mabaya ya ofisi ilhali 32 waliunga mkono mashtaka ya kukiuka sheria za uhalifu.
Hoja ya kumuondoa mamlakani Naibu Gavana huyo iliwasilishwa na kiranja wa wengi katika bunge la Seneti Dkt. Boni Khalwale.
Japo mashtaka ya uhalifu hayakubainishwa, kulikuwa na uwezekano kwamba Naibu Gavana huyo alipokea hongo.
Bunge la kaunti ya Kisii lilisema kuwa Dkt. Monda alipokea hongo ya shilingi 800,000 kutoka kwa mkazi wa kaunti hiyo ili amsaidie kumtafutia mwanawe ajira.
Awali, Dkt. Monda alikanusha mashtaka yote dhidi yake.