Bunge la seneti leo Jumatano, litaanza vikao vya kusikiliza na kuamua hoja iliyopendekezwa ya kutaka kuondolewa mamlakani kwa naibu gavana wa kaunti ya Kisii Robert Monda.
Hii ni baada ya bunge hilo kukubaliana kufanyia marekebisho vikao vyake vya siku ya Jumatano na Alhamisi, ambapo itakuwa siku ya mwisho ya seneti kupiga kura ili kuamua iwapo litaunga mkono au kupinga hoja ya kubanduliwa mamlakani kwa Monda.
Hoja iliyoidhinishwa ya kufanyia marekebisho vikao vya bunge hilo ilipendekezwa na kiongozi wa walio wengi, Aaron Cheruiyot.
Maseneta watahudhuria vikao vyote vya asubuhi na alasiri siku hizo mbili.
Naibu huyo wa gavana aling’atuliwa mamlakani tarehe 29 mwezi Februari mwaka huu na wawakilishi wadi wa kaunti ya Kisii kwa madai ya matumizi mabaya ya mamlaka na ulaji rushwa.