Kamati ya Michezo katika Bunge la Kitaifa imetishia kumwekea vikwazo Katibu wa Wizara ya Michezo Peter Tum, baada yake kukosa kufika mbele yake kujibu maswali ya uwajibikaji katika Wizara yake.
Kamati hiyo inayoongozwa na Mbunge wa Webuye Magharibi Dan Wanyama, imekerwa na hatua ya Katibu Tum kupuuza kufika yake, kujibu maswali ikiwemo kucheleweshwa kwa ujenzi wa akademia za michezo na viwanja nchini.
Wanyama amesema kuwa huenda kamati ikalazimika kumtoza faini ya shilingi nusu milioni kama adhabu.
“Katibu ana hulka ya kukwepa vikao vyetu muhimu kujibu maswali ya ucheleweshaji ujenzi wa akademia 25 za michezo katika maeneo Bunge kadhaa ndani ya awamu ya kwanza ya mradi huo.”akasema Wanyama
Wanayama ameonya kuwa kamati hiyo haitasita kumchukulia hatia Tum endapo hataitikia mwito wa mwisho wa kufika mbele ya kamati Jumanne ijayo.
“Tumemwalika Jumanne ijayo kwa mara ya mwisho na endapo hatafika tutatumia mamlaka tuliyo nayo na kumwadhibu Tum.”akasisitiza Wanyama
Kulingana na Wanyama ucheleweshwaji wa ujenzi wa akademia hizo kunamchafulia sifa Rais Ruto, aliyekuwa ametoa ahadi hiyo na kuonekana mwongo jambo ambalo hatakubali kamwe .
Mbunge wa Teso Kusini Catherine Amayo ameongeza kuwa ujenzi wa akademia hizo katika maeneo bunge kadhaa nchini, kulikuwa kumeleta msisimko miongoni mwa vijana lakini ametamaushwa na kucheleweshwa kwa utekelezaji wake.
Naye Mbunge wa Bomet Mashariki Richard Yegon amesema hatua ya Katibu Tum kukosa kufika mbele yake ni dharau kubwa.
Mbunge wa Matungulu Stephen Mule amemtaka Rais kumpiga kalamu Katibu huyo, akisema kukosa kufika mbele ya kamati kunaashiria utepetevu wake katika Wizara ya Michezo.
Aliongeza kuwa Wabunge wa kamati hiyo walitoka kwenye likizo ili kumwalika Tum ajibu maswali na badala yake akasusia.
Mwakilishi wa akina mama kaunti ya Marsabit Naomi Waqo, amesema vijana wanataabika kutokana na kucheleweshwa kwa ujenzi wa viwanja na Akademia na kumtaka Katibu kumakinika katika kazi yake kwa kufika mbele ya kamati hiyo.