Mwanamuziki Brown Mauzo ametangaza kwamba yeye na mama ya watoto wake Vera Sidika wameachana.
Kupitia akaunti yake ya Instagram, Mauzo alichapisha ujumbe kwa marafiki na wafuasi wao akielezea kwamba yeye na Sidika wameamua kuachana hata ingawa muda wao pamoja umekuwa na mengi mazuri.
“Tumeafikia uamuzi kwamba ni bora tutengane kwa manufaa yetu na ya watoto wetu wawili Asia Brown na Ice Brown.” alisema Mauzo kupitia taarifa hiyo.
Aliomba umma uwaelewe na uheshimu maisha yao ya kibinafsi wanapopitia kipindi hiki.
Mauzo na Sidika walioana rasmi Oktoba 2020 na wamejaliwa watoto wawili Asia Brown aliyezaliwa Oktoba 2021 na Ice Brown aliyezaliwa yapata miezi mitatu iliyopita.
Mwanzo wa mwezi Juni mwaka huu, Vera Sidika ambaye ni mmoja wa wahusika wa kipindi cha “Real Housewives of Nairobi” alionyesha cheti cha ndoa kwenye kipindi hicho kama ithibati ya ndoa yake na Brown Mauzo.
Hatua hiyo alisema ililenga kunyamazisha wote ambao walikuwa wanatilia shaka uhusiano wao iwapo kweli walikuwa kwenye ndoa.
Sidika hajasema lolote kuhusu utengano uliotangazwa na baba ya watoto wake.
View this post on Instagram