Jana Januari 1, 2025, mwanamuziki wa Congo, Bozi Boziana, aliandaa onyesho kubwa la burudani katika Ukumbi wa New Kiduli, Magomeni Kanisani, jijini Dar es Salaam.
Onyesho hilo lilihusisha bendi ya muda mrefu ya Twanga Pepeta, ambayo iliongeza ladha ya burudani ya hali ya juu.
Katibu Mtendaji wa BASATA, Dkt. Kedmon Mapana, alihudhuria onyesho hilo kama mgeni rasmi na kutoa hotuba iliyojaa pongezi na hamasa kwa wadau wa muziki wa dansi nchini Tanzania.
Alipongeza chama cha muziki wa densi nchini Tanzania – CHAMUDATA kwa juhudi zao za kukuza sanaa ya muziki wa dansi na kuwakumbusha wapenzi wa muziki kuhusu tukio kubwa lijalo.
Tamasha hilo litaandaliwa Februari Mosi huko Leaders’ Club, jijini Dar es Salaam na linatarajiwa kuwa la kipekee na kuaandika historia mpya katika muziki wa dansi nchini Tanzania.
Bendi maarufu, ikiwemo Twanga Pepeta zitashiriki na ni fursa adimu kwa wapenzi wa muziki kufurahia burudani ya kiwango cha juu.”
Tamasha hilo limepatiwa jina la ‘Kadancee la Mama Samia’ limeandaliwa kwa ushirikiano wa Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo na Shirikisho la Muziki Tanzania.
Kulingana na Mapana tamasha hilo ni la kutoa heshima kwa Rais Samia Suluhu Hassan, ambaye amekuwa mstari wa mbele katika kuunga mkono sekta ya sanaa na michezo.
“Tunaomba kila mmoja ajitokeze kwa wingi kufurahia burudani hii ya kihistoria.” alialika Mapana.