Bobi Wine aondoka hospitalini

Marion Bosire
2 Min Read

Mwanamuziki na mwanasiasa Bobi Wine aliruhusiwa kuondoka hospitalini jana alikopelekwa Jumanne baada ya kujeruhiwa mguu katika makabiliano na maafisa wa polisi.

Awali wasaidizi wake walitangaza kwamba alikuwa amepigwa risasi lakini baadaye maafisa wa polisi nchini Uganda walifafanua kwamba aligongwa na kopo la kitooza machozi.

Siku ya Jumanne Wine alikuwa akielekea Bulindo kushauriana na mawakili wake, umbali wa kilomita 20 kaskazini mwa mji mkuu wa nchi hiyo, Kampala kisa hicho kilipotokea.

Kulingana na Meya wa jiji kuu la Kampala, Bobi alifanyiwa upasuaji ili kuondoa vipande vya kopo hilo vilivyokuwa vimeingia kwenye mguu wake.

Meya huyo kwa jina Erias Lukwago alielezea kwamba Wine aliruhusiwa kuondoka kwenye hospitali ya Nsambya kufuatia kuimarika kwa hali yake.

Lakini msemaji wa chama cha Bobi Wine National Unity Party NUP Joel Ssenyonyi ana usemi tofauti na wa Meya Lukwago ambapo alielezea kwamba waliomba madaktari wamruhusu Wine kuondoka hospitalini.

Kulingana naye, walikuwa wamepokea ripoti kuhusu maafisa wa polisi ambao hawakuwa wamevaa sare waliokuwa wakitaka wapatiwe stakabadhi za Wine na waingie kwenye chumba alichokuwa amelazwa.

Maafisa wa polisi walionekana wakiwa wamezingira hospitali hiyo na kudhibiti trafiki kwenye barabara zinazoelekea humo ambapo msemaji wa polisi Rusooke Kituuma alisema kwamba nia ya kuweka maafisa hao huko ni kuhakikisha usalama.

Wine sasa atakamilisha matibabu yake nyumbani huko Magere.

Share This Article