Binti ya Angelina Jolie na Brad Pitt aanza mchakato wa kuondoa jina ‘Pitt’

Marion Bosire
2 Min Read

Binti ya waigizaji na waandaaji filamu wa Marekani Angelina Jolie na Brad Pitt kwa jina “Shiloh Nouvel Jolie-Pitt” amewasilisha kesi katika mahakama moja huko Los Angeles ya kutafuta idhini ya kuondoa jina “Pitt” kwenye jina lake.

Shiloh ambaye pia ni mwigizaji, anataka kubadili jina lake ili liwe “Shiloh Jolie” kupitia kesi hiyo aliyoiweka mahakamani Mei 27, 2024, siku ya kuzaliwa kwake na ndiyo siku alitimiza umri wa miaka 18.

Angelina Jolie alianzisha mchakato wa kumtaliki Brad Pitt Septemba 2016, lakini kufikia sasa haijakamilika na hawajaafikia namna ya kugawana mali.

Shiloh ndiye mtoto wa tatu kati ya watoto sita wa Angelina Jolie na Brad Pitt, na amekuwa wa pili kati ya watoto hao kuondoa jina la babake kwenye jina lake.

Mwanzo wa mwaka huu, dadake Shiloh kwa jina Vivienne wa umri wa miaka 15 aliondoa jina “Pitt” kwenye jina lake alipojisajili kwa mpango wa Playbill kwa uaandaaji wa “The Outsiders” kwenye Broadway.

Mwaka jana binti ya Brad na Angelina mkubwa aitwaye Zahara alijitambulisha kama “Zahara Marley Jolie” alipokuwa anajiunga na kundi la Alpha Kappa Alpha katika taasisi ya Spelman.

Shiloh ndiye ametumia njia ya kisheria kubadili jina lake.

Angelina Jolie na Brad Pitt walifunga ndoa mwezi Agosti mwaka 2014, na Jolie alianzisha mipango ya talaka mwaka 2016 baada ya kile anachokitaja kuwa hatua ya Pitt ya kumshambulia yeye na wanao wakiwa kwenye ndege.

Pitt anasemekana kumtukana Jolie na kummiminia pombe kwenye ndege hiyo iliyokuwa imewabeba kutoka Ufaransa kuelekea Los Angeles, Marekani.

Share This Article