Bill Cosby ameshtakiwa tena kwa dhuluma za kimapenzi, visa vinavyosemekana kutokea miaka ya awali.
Janice Dickinson na Lili Bernard ni kati ya wanawake tisa ambao wamemshtaki mwigizaji huyo mkongwe kwa kuwadhulumu kimapenzi.
Cosby anasemekana kutekeleza makosa hayo huko Nevada kati ya mwaka 1979 na 1992.
Wanawake hao wanadai kwamba walitendewa makosa hayo na Bwana Cosby kwenye chumba alichokuwa akikaa katika hoteli ya Las Vegas.
Lili, ambaye aliwahi kuigiza kwenye kipindi cha “The Cosby Show” anaelezea kwamba Cosby alimpangia safari kutoka New York hadi Nevada mwaka 1990 akisingizia kwamba alikuwa ahudhurie mkutano na watayarishaji filamu kutoka Hollywood.
Lili alipofika Las Vegas, Cosby alimwambia kwamba watayarishaji filamu wa Hollywood hawangeweza kufika lakini akampeleka kwenye chumba chake kwa kile alichokitaja kuwa ushauri lakini akampa kinywaji kilichomfanya ahisi usingizi na asijijue.
Anasema alizimia na alipotanabahi, akajipata uchi karibu na Cosby ambaye pia alikuwa uchi.
Anasema Cosby alimbaka hata baada yake kumwambia wazi kwamba hakutaka kushiriki tendo la ndoa naye.
Katika chumba hicho hicho, Janice anasema Cosby alimwalika ili akamtembeze mwaka 1982 ambapo wangezungumzia uwezekano wa kumpa nafasi ya kuigiza kwenye kipindi chake.
Walikwenda kupata chajio ambapo alilalamikia maumivu ya hedhi na Cosby akampa dawa ya kumeza ambayo alimwambia ingemsaidia kupunguza maumivu.
Janice vile vile alihisi usingizi na kutoweza kujitambua baada ya kumeza tembe hiyo na anasema Cosby alichukua fursa hiyo akampeleka chumbani alikombaka.
Anasema alijaribu kupigana naye ili kuzuia unyama aliotendewa lakini hakufanikiwa.
Cosby amekuwa akishtakiwa kwa makosa ya dhuluma za kingono na wanawake wapatao 60, visa ambavyo vilitokea miaka mingi iliyopita lakini huenda vikakubalika kama mashtaka kwa sababu majimbo kadhaa nchini Marekani yanabadili sheria za kushughulikia dhuluma za kingono.