Bien kuandaliwa tamasha na waandalizi wa tuzo za Trace

Bien ndiye mwanamuziki pekee wa Kenya ambaye ameteuliwa kuwania tuzo za Trace mwaka huu.

Marion Bosire
2 Min Read

Bien Aime ambaye ndiye mwanamuziki pekee wa Kenya ameteuliwa kuwania tuzo za Trace mwaka 2025, ataandaliwa tamasha na waandalizi wa tuzo hizo kesho Alhamisi jijini Nairobi.

Awamu ya pili ya tuzo za Trace itaandaliwa huko Zanzibar nchini Tanzania na waandalizi wanatekeleza ziara ya kusherehekea walioteuliwa kuwania tuzo katika eneo zima la Mashariki ya Afrika.

Kulingana na tangazo lililopachikwa kwenye akaunti ya Instagram ya tuzo za Trace, tamasha hilo la Bien litaandaliwa katika baa ya Alloy kwenye jumba la kibiashara la Sarit na litaanza zaa nne usiku.

Msanii huyo wa kundi la Sauti Sol ameteuliwa kuwania tuzo ya msanii bora wa Mashariki ya Afrika pamoja na Diamond Platnumz, Harmonize, Zuchu, Nandy na Marioo wote wa Tanzania.

Wengine ni Joshua Baraka wa Uganda na Rophnan wa Ethiopia.

Hafla ya kutoa tuzo hizo pamoja na kongamano la Trace zimepangiwa kuandaliwa Februari 24 hadi 26, 2025 huko Zanzibar nchini Tanzania.

Awamu ya kwanza kabisa ya tuzo hizo pamoja na kongamano la Trace viliandaliwa Oktoba 2023, jijini Kigali nchini Rwanda.

Wakati huo wasanii wa Kenya walioteuliwa kuwania tuzo ni pamoja na Nadia Mukami katika kitengo cha mwanamuziki bora wa kike na kile cha mwanamuziki bora wa Afrika Mashariki, Janet Otieno kitengo cha msanii bora wa nyimbo za injili na Khaligraph Jones katika kitengo cha mwanamuziki bora wa Afrika Mashariki.

Website |  + posts
Share This Article