Beyonce aliridhisha sana kwenye tumbuizo lake la muda wa mapumziko wa mchuano wa soka wa ligi ya kitaifa NFL, zawadi bora zaidi ya Krismasi kwa mashabiki waliokuwepo.
Mchuano huo ulikuwa kati ya timu za Houston Texans na Baltimore Ravens, katika uga wa NRG.
Mwimbaji huyo aliwapa mashabiki mpangilio mzuri wa miziki uliojumuisha nyimbo za Krismasi na nyingine kutoka kwa albamu yake ya hivi karibuni ya ‘Cowboy Carter’ onyesho lililopeperushwa moja kwa moja kwenye jukwaa na Netflix.
Aliimba nyimbo kama 16 Carriages, Spaghetti, Jolene na Texas Hold Em akisaidiwa na wanamuziki wengine kama Shaboozey na Post Malone.
Bendi pia ilihusika huku wacheza densi nao wakifanya haki wakiwa wamevaa mikanda yenye rangi za bendera ya Marekani na jina la albamu ya Beyonce “Cowboy Carter”.
Beyonce au Queen Bey kama anavyorejelewa na wengi alisaidiwa jukwaani pia na binti yake Blue Ivy, ambaye alicheza akisonga taratibu hadi akafika karibu kabisa na mamake.
Mchuano huo wa soka uliishiwa kwa ushindi wa 31-2 uliopendelea timu ya Baltimore Ravens.