Joshua Belet amewaongoza Wakenya kutwaa nafasi tatu za kwanza katika makala ya 47 ya mbio za kila mwaka za Amsterdam Marathon zilizoandaliwa mapema Jumapili nchini Uholanzi.
Belet ametimka mbio hizo kwa muda wa saa 2, dakika 4 na sekunde 18 akifuatwa na Cybrian Kotut kwa saa 2, dakika 4 na sekunde 33, huku Bethwel Chumba akimaliza wa tatu kwa saa 2, dakika 4 na sekunde 35.
Wanariadha wa Ethiopia walinyakua nafasi mbili za kwanza upande wa vipusa, Meseret Belete akiongoza kwa saa 2, dakika 18 na sekunde 19 akifuatwa na Meseret Abebayehu, aliyetumia saa 2, dakika 19 na sekunde 47 huku Dorcas Tuitoek wa Kenya akiibuka katika nafasi ya tatu kwa saa 2 na dakika 20.