Chama cha UDA kimewahakikishia Wakenya kwamba bei za mafuta hazitapanda licha ya mgogoro unaoendelea Mashariki ya Kati.
Aidha, chama hicho kimesema bei hizo hazitaathiriwa na uagizaji ulioripotiwa wa mafuta ya kiwango cha chini nchini.
“Ili kuelezea bayana matukio ya hivi karibuni, tunawahakikishia Wakenya kwamba hawataadhibiwa katika ununuzi wa mafuta kutokana na uagizaji huu wa mafuta wenye kusudi mbaya,” alisema Katibu Mkuu wa UDA Hassan Omar.
“Katika mapitio ya bei mpya zijazo za mafuta, Mamlaka ya Kudhibiti Nishati na Bidhaa za Mafuta, EPRA itadumisha mpangokazi wa bei za mafuta wa Serikali hadi Serikali, ambao umesalia thabiti, wenye usawa, na wa kutegemewa.”
Omar akielezea kuwa mpangokazi huo unatoa ulinzi mwafaka wa mafuta thabiti, usambazaji thabiti na usalama wa nishati kote nchini.
Na huku ripoti za uagizaji mafuta ya kiwango cha chini zikienea kila pembe, Katibu Mkuu huyo alisema hatua thabiti zimechukuliwa ili kudhibiti hatari zinazotokana na uagizaji huo, ikiwa ni pamoja na upimaji wa shehena ya mafuta hayo.
Aliongeza kuwa matokea ya upimaji huo yatawekwa wazi ili kuhakikisha uwazi.
Kashfa ya uagizaji mafuta ilikuwa kiini cha kujiuzulu kwa maafisa wakuu katika sekta ya nishati Jumamosi iliyopita.
Wao ni Katibu wa Idara ya Petroli Mohamed Liban na Wakurugenzi Wakuu Joe Sang wa Kenya Pipeline na Daniel Kiptoo wa EPRA.
Rais William Ruto ameapa kukabiliana vikali na matapeli katika sekta ya mafuta nchini.