Barchok, Wangamati washtakiwa kwa tuhuma za ufisadi

Magavana hao wawili wanakabiliwa na mashtaka mbalimbali ya ufisadi ikiwa ni pamoja na ulanguzi wa fedha. Mahakama itatoa mwelekeo wa kesi dhidi yao Septemba 17.

Martin Mwanje
1 Min Read
Gavana wa zamani wa Bungoma Wycliffe Wangamati (kushoto) akiwa na washirika wake mahakamani

Gavana wa Bomet Hillary Barchok na Gavana wa zamani wa Bungoma Wycliffe Wangamati leo Jumanne walifikishwa mahakamani ili kujibu mashtaka ya ufisadi yanayowakabili.

Wawili hao walifikishwa katika Mahakama ya Kupambana na Ufisadi ya Milimani wakiwa wameandamana na washirika wao.

Wangamati alikuwa wa kwanza kufikishwa mahakamani akiandamana na washirika wake 18, wakiwemo jamaa zake na wanakandarasi.

Wote hao wanakabiliwa na mashtaka 27 ya ufisadi yanayojumuisha utoaji tata wa zabuni za ujenzi wa barabara wakati wa utawala wa Gavana huyo wa zamani.

Wote hao walikanusha mashtaka huku mahakama ikimwachilia Wangamati kwa dhamana ya shilingi milioni 5.

Washirika wake kwenye kesi hiyo walipewa dhamana ya shilingi milioni 10.

Kisha Gavana wa kaunti ya Bomet Hillary Barchok akiandamana na mshirika wake Evans Kipkoech walifikishwa kizimbani.

Wawili hao wakikanusha mashtaka ya ufisadi dhidi yao na kuachiliwa kwa dhamana ya shilingi milioni 15 na milioni 5 mtawalia.

Mahakama itatoa mwelekeo wa kesi hizo mbili Septemba 17 mwaka huu.

 

 

 

 

Website |  + posts
Share This Article