Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa, UNSC leo Jumatatu linapiga kura kuamua kuhusu wazo la kutuma kikosi cha polisi cha kimataifa nchini Haiti kwa muda wa mwaka mmoja.
Lengo la wazo hilo ni kuimarisha usalama katika nchi hiyo ambayo imekumbwa na ghasia za makundi yaliyojihami ili kuhakikisha uchaguzi unaandaliwa.
Marekani katika mawasilisho yake kwa baraza hilo imeteua Kenya kuongoza kikosi hicho ambacho hakitakuwa cha Umoja wa Mataifa na kitafadhiliwa na nchi ambazo zitajitolea.
Inapendekeza pia kwamba muda wa kuhudumu wa kikosi hicho uwe mwaka mmoja na fursa ya kuongeza muda huo kwa miezi tisa.
Kikosi hicho kitasaidia kikosi cha polisi cha Haiti kujiimarisha.
Haiti ina maafisa wa polisi wapatao elfu 10 huku idadi ya watu nchini humo ikiwa zaidi ya milioni 11.
Maafisa wa polisi watakaotumwa nchini Haiti watasaidia kulinda sehemu za umma kama barabara, vituo vya usafiri na viwanja vya ndege. Maeneo hayo yanadhibitiwa na magenge hatari.
Iwapo wazo hilo litaidhinishwa na UNSC, basi litatoa fursa ya hatua za haraka za kustawisha Haiti.
Iwapo litapitishwa, nchi ya kuongoza mpango huo ambayo ni Kenya itahitajika kufahamisha baraza hilo kuhusu malengo ya mpango huo, sera za kuudhibiti, mahitaji ya kifedha na masuala mengine muhimu.