Baraza la Mawaziri lakutana, laangazia hali ya usalama nchini

Martin Mwanje
2 Min Read
Baraza la Mawaziri limekutana leo Alhamisi katika Ikulu ya Nairobu na kutaarifiwa juu ya hali ya usalama nchini kufuatia maandamano ambayo yamekuwa yakiendelea kwa siku kadhaa.
Mkutano wa mawaziri hao uliofanyika katika Ikulu ya Nairobi uliongozwa na Rais William Ruto. Ulitaarifiwa kuwa ingawa mandamano yalianza ili kupinga Mswada wa Fedha 2024, wahalifu na wanasiasa walitumia fursa hiyo kuendeleza ajenda zao.
“Makundi hayo mawili katika muda wa wiki mbili yamewasababishia hofu Wakenya wanaoishi katika maeneo ya miji na kusababisha vifo, uharibifu wa majengo ya serikali kuu na za kaunti, miundombinu, magari na biashara,” ilisema taarifa kutoka kwa Idara ya Mawasiliano ya Rais, PCS.
Kutokana na tishio kwa bunge, Mahakama ya Juu na miundombinu mingine, Baraza la Mawaziri lilitaarifiwa kuwa vyombo vyote vya usalama likiwemo jeshi, vilitumwa ili kurejesha utulivu.
Baraza hilo kadhalika lilitaarifiwa kuwa vyombo vya usalama vimetuliza hali na vinaendelea kufuatilia mambo yalivyo.
Mawaziri waliwapongeza maafisa wa usalama wakisema walitekeleza majukumu yao kitaalam katika hali ngumu zaidi. Kadhalika, walisema vyombo vya usalama vilifanya kazi nzuri katika kulinda nchi dhidi ya watu waliochochea machafuko.
Rais Ruto alisema serikali kwa sasa inaangazia kuanzisha mustakabali mpya wa taifa, akisema mabadiliko makubwa yanapaswa kufanywa ili kuwiana na siku mpya zijazo.
Kuhusu afisa yeyote ambaye hakuzingatia sheria katika utendaji kazi wake, Baraza la Mawaziri lilisema maafisa kama hao watakabiliwa kwa mujibu wa taratibu za sheria na taasisi zilizokabidhiwa mamlaka ya kushughulikia hilo.
Baraza hilo kadhalika lilitoa wito wa kuchukuliwa kwa hatua dhidi ya wale wote waliojihusisha katika visa vya uhalifu ikiwa ni pamoja na uporaji na uchomaji wa mali.
Kuhusiana na Mswada wa Fedha ulioondolewa, Rais Ruto alisema Wizara ya Fedha inaandaa upya bajeti ili kuwiana na uhalisia mpya wa mambo.
Share This Article
Leave a Comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *