Baraza la Mawaziri laidhinisha kubuniwa kwa jopokazi la kuangazia mauaji ya wanawake

Martin Mwanje
2 Min Read
Baraza la Mawaziri limeidhinisha kubuniwa kwa jopokazi la rais litakalobuni mpango madhubuti wa kukabiliana na mauaji ya wanawake nchini. 
Jopokazi hilo litafanya mashauriano na viongozi wa kidini, wazazi, shule, asasi za usalama na washikadau wengine kutambua mianya iliyopo katika sheria, utekelezaji wa sheria hiyo na maadili ya jamii yanayochangia kuongezeka kwa mauaji hayo.
Aidha jopokazi hilo litachapishwa kwenye gazeti rasmi la serikali likiwa na mamlaka mahususi ya kazi yake na kupewa jukumu la kutoa mapendekezo ya kufanyiwa kazi ndani ya siku 90.
Mkutano wa Baraza la Mawaziri wa leo Jumanne uliofikia uamuzi huo uliongozwa na Rais William Ruto na ulifanyika katika Ikulu ya Nairobi.
Huo ndio mkutano wa mwisho wa Baraza la Mawaziri kufanyika mwaka huu unaoelekea kumalizika.
Hatua ya Baraza la Mawaziri inakuja wakati kumekuwa na visa vingi vya mauaji ya wanawake vilivyoripotiwa nchini katika siku za hivi karibuni.
Mauaji hayo yalisababisha taasisi mbalimbali ikiwa ni pamoja na Chama cha Mawakili Wanawake, FIDA kutaka yatajwe kuwa janga la kitaifa.
Awali, Huduma ya Taifa ya Polisi ilitangaza kuuawa kwa wanawake wasiopungua 90 katika kipindi cha miezi mitatu.
Rais Ruto amezitaka asasi za usalama kuwachukulia hatua kali wale wote wanaohusika katika mauaji ya wanawake nchini na kutaka uovu huo kukomeshwa mara moja.
Share This Article
Leave a Comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *