Baraza la Mawaziri limeidhinisha kuanzishwa kwa kamati maalum ya kushughulikia madeni ya serikali.
Kamati hiyo ya kuthibitisha fedha zinazosubiriwa, itakabidhiwa jukumu la kukagua madeni katika kipindi kati ya 2005 na 2022.
Katika kikao kilichoongozwa na Rais William Ruto katika Ikulu ya Nairobi, Baraza la Mawaziri lilibainisha kuwa malipo ya madeni yamesalia kuwa swala gumu.
Madeni ya serikali ya kitaifa kuanzia Juni, 2005 hadi Juni, 2022 yanafikia shilingi bilioni 481 huku kaunti zikidaiwa shilingi bilioni 159.9.
Kamati hiyo itajumuisha Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Idara ya Barabara, Idara ya Ujenzi, Idara ya Nyumba na Maendeleo ya Miji na Mamlaka ya Kudhibiti Ununuzi wa Umma.
Tume ya Maadili na Kupambana na Ufisadi, Chama cha Wanasheria Nchini, LSK, Taasisi ya Wahandisi wa Kenya na Taasisi ya Wahasibu wa Umma Walioidhinishwa Nchini pia zitakuwa sehemu ya kamati hiyo.
Kamati itachunguza na kuwasilisha taarifa za muda kwa Waziri wa Hazina ya Kitaifa baada ya kuthibitishwa. Serikali itawajibika na swala husika.
Hatua hiyo inalenga kuweka uadilifu wa malipo ya madeni yote na kuzilinda biashara ndogo ndogo dhidi ya kusambaratika.
Muhimu zaidi, kamati hiyo itapendekeza utaratibu wa kukomesha hali ya kukosekana kwa fedha siku zijazo.
Ilikubalika kuwa kamati hiyo itawasilisha ripoti yake ya mwisho ndani ya mwaka mmoja.