Baraza la kitaifa la Kiswahili litabuniwa karibuni, asema Aisha Jumwa

Tom Mathinji
2 Min Read
Waziri wa masuala ya jinsia, utamaduni, sanaa na turathi Aisha Jumwa.

Huku Kenya ikijiandaa kuungana na ulimwengu kuadhimisha siku ya Kiswahili duniani Julai 7, 2024, mipango imeratibiwa kuhakikisha Baraza la kitaifa la Kiswahili linabuniwa na kutambuliwa kisheria. 

Akizungumza katika kaunti ya Mombasa leo Ijumaa wakati wa kongamano la siku tatu la lugha ya Kiswahili, waziri wa masuala ya jinsia, utamaduni, sanaa na turathi Aisha Jumwa, alidokeza kuwa wizara yake imewasilisha waraka wa Baraza la Mawaziri kwa Mwanasheria Mkuu kutambua baraza hilo la Kiswahili.

Mnamo Julai 3, 2024 mataifa wanachama wa Baraza kuu la Umoja wa Mataifa, UNGA yalipitisha azimo lililowasilishwa na Kenya na Tanzania kwa niaba ya nchi za bara Afrika, kwamba Julai 7 itakuwa Siku ya Kiswahili Duniani.

Azimio hilo lilitambua wajibu muhimu unaotekelezwa na lugha ya Kiswahili katika kuleta amani, umoja, maendeleo ya kijamii na kiuchumi, tofauti za utamaduni pamoja na kubuni uhamasishaji na kukuza mazungumzo miongoni mwa watu.

Waziri Jumwa alisema baraza hilo limepewa jukumu la kukuza lugha ya Kiswahili hapa nchini, ambayo ni nguzo inayounganisha mataifa wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki.

Shirika la Elimu, Sayansi na Utamaduni la Umoja wa Mataifa ‘UNESCO’, lilitangaza Julai 7 kuwa siku ya lugha ya Kiswahili duniani mnamo mwaka-2022.

Kiswahili ni miongoni mwa lugha 10 zinazozungumzwa zaidi duniani, wengi wa wazungumzaji wakitoka bara Afrika.

TAGGED:
Share This Article
Leave a Comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *