Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa limepitisha kwa wingi azimio lisilo la lazima la kutaka kusitishwa mara moja kwa mapigano ya Gaza kwa maslahi ya kibinadamu.
Nchi wanachama 153 zilipiga kura ya ndio, 10 zilipinga na 23 zilijizuia.
Balozi wa Palestina katika Umoja wa Mataifa alisema kura ya kuunga mkono usitishaji vita huko Gaza ni “siku ya kihistoria kwa kuzingatia ujumbe wenye nguvu uliotumwa kutoka kwa mkutano mkuu”.
“Ni jukumu letu sote kuendelea na juhidi hizi hadi tuone mwisho wa uchokozi huu dhidi ya watu wetu,” Riyad Mansour alisema.
Hili lilikuwa jaribio la pili la Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa ambalo mwezi Oktoba lilitoa wito wa “maafikiano ya kibinadamu” katika azimio lililopitishwa kwa kura 121 za kuunga mkono, 14 za kupinga na 44 za kujizuia.
Marekani, Paraguay, Austria na Israel walikuwa miongoni mwa wanachama 10 waliopiga kura kupinga azimio hilo.
Huku hayo yakijiri, Wizara ya Afya ya Gaza, ambayo inasimamiwa na Hamas, inasema zaidi ya watu 18,400 wameuawa na wengine 50,000 wamejeruhiwa tangu kuanza kwa mashambulio ya Israel.
Umoja wa Mataifa na mashirika ya misaada yamekuwa yakinakili baadhi ya mambo yanayozuia kutibiwa kwa waliojeruhiwa.