Bangi ya thamani ya shilingi milioni 12 yateketezwa Marsabit

Tom Mathinji
1 Min Read
Kamishna wa Marsabit James kamau aongoza zoezi la uteketezaji bangi.

Serikali ya kaunti ya Marsabit imeteketeza kilo 521 za bangi ya thamani ya shilingi milioni 12, katika juhudi za kuimarisha vita dhidi ya ulanguzi wa mihadarati katika kaunti hiyo.

Shughuli hiyo iliyoongozwa na kamishna wa kaunti ya Marsabit James Kamau, ilitekelezwa katika eneo la Segel, baada ya idhini kutoka kwa Mahakama ya Marsabit, baada ya kukamilika kwa kesi zilizohusiana na mihadarati hiyo.

Kamishna huyo alisema hawatalegeza kamba katika vita dhidi ya ulanguzi wa mihadarati katika eneo hilo.

Bangi hiyo inajumuisha kilo 455 zilizonaswa kutoka kwa aliyekuwa mwaniaji wa urais katika uchaguzi wa mwaka 2013  Jeffar Isaak Sora, katika barabara ya Moyale – Marsabit.

Maafisa wa usalama katika siku za hivi karibuni wamenasa bangi zilizokuwa zikisafirishwa kupitia barabara ya Moyale- Marsabit.

Maafisa wa polisi waliokuwa wakishika doria walinasa lori lililokuwa likisafirisha bangi ya thamani ya shilingi milioni 35,katika kituo cha Anona kwenye barabara ya Moyale – Marasabit

Mnano Oktoba 4,2024, maafisa wa polisi walinasa mifuko 12 ya bangi katika eneo la Burgabo katika barabara ya Moyale- Marsabit.

TAGGED:
Share This Article