Maafisa wa upelelezi kutoka Kitengo cha Kupambana na Dawa za Kulevya, ANU katika eneo la Bonde la Ufa wamenasa bangi ya thamani ya shilingi milioni 8.1.
Wamekamata pia mshukiwa wa ulanguzi wa dawa za kulevya baada ya msako mkali katika Barabara Kuu ya kutoka Eldoret kuelekea Nakuru.
Tukio hilo ni la jana tarehe 14 Machi 2026, wakati maafisa waliokuwa kwenye doria ya kawaida walisimamisha gari aina ya Toyota Voxy ya rangi ya bluu, nambari ya usajili KCS 496B, baada ya kulitia shaka.
Dereva alikaidi amri ya kusimama na kuongeza mwendo kwa kasi, jambo lililosababisha afuatwe kwa kasi kuelekea eneo la Kaptembwa.
Wakati wa msako huo, maafisa walifanikiwa kupunguza hewa ya tairi la mbele la upande wa kulia la gari hilo.
Licha ya uharibifu huo, mshukiwa aliendelea kuendesha gari kuelekea eneo la 140 kabla ya kulitelekeza katika kiwanja wazi karibu na Kituo cha Polisi cha Kaptembwa na kujaribu kutoroka.
Dereva huyo, aliyetambuliwa kama David Muraya wa umri wa miaka 35, alizingirwa haraka na kukamatwa na maafisa waliokuwa wakimfuatilia.
Upekuzi uliofanywa ndani ya gari ulisababisha kupatikana kwa magunia kumi na matatu yaliyokuwa na majani makavu ya kijani yanayoshukiwa kuwa bangi, yenye uzito wa takriban kilo 272 na thamani ya takriban shilingi milioni 8,160,000.
Mshukiwa bado anazuiliwa na polisi akisubiri kufikishwa mahakamani kesho Jumatatu, tarehe 16 Machi 2026.