Balozi Amina Mohamed leo Disemba 6, 2023 amejiunga rasmi na bodi ya usimamizi ya shirika la kimataifa la amani yaani International Organisation for Peacebuilding maarufu kama Interpeace.
Bodi hiyo ndiyo kiungo kikuu cha maamuzi katika shirika hilo ambalo jukumu lake kuu ni kuzuia migogoro na kuhakikisha amani ya kudumu katika maeneo mbali mbali ulimwenguni.
Tajriba ya waziri huyo wa zamani katika masuala ya diplomasia na maendeleo itakuwa ya thamani kwa shirika hilo linapotafuta amani na usalama.
Shirika la Interpeace limekuwepo kwa miaka 27 sasa na limehudumu katika maeneo yanayoshuhudia mafarakano kama vile sehemu za bara Afrika, Mashariki ya kati, bara Asia, Uingereza na Latin America.
Wanachama wa bodi ya usimamizi ya shirika la Interpeace ni watu maarufu kutoka kwa serikali, kimataifa na sekta ya biashara.
Serikali ya Switzerland ambapo afisi kuu za shirika hilo ziko, nayo ina nafasi moja kwenye bodi sawasawa na mwakilishi mmoja wa umoja wa mataifa.