Bahati alalamikia utawala wa wanamuziki wa Tanzania nchini Kenya

Marion Bosire
2 Min Read

Mwanamuziki Kelvin Kioko maarufu kama Bahati analalamika kufuatia kupendeka kwa muziki wa wanamuziki wa nchi jirani Tanzania nchini Kenya.

Kupitia akaunti yake ya Instagram, msanii huyo alisema amelazimika kutoa sauti kuhusu suala hilo na ni kutokana na upendo alionao kwa wanamuziki wenzake nchini.

Alichapisha picha za nyimbo pendwa kwenye majukwaa ya mitandaoni kama vile YouTube, Boomplay, itunes na hata redio na runinga za humu nchini, ambapo nambari moja hadi kumi ya nyimbo zinazopendwa nchini ni za waimbaji wa Tanzania.

“Tumeacha Jirani analala Hadi Na Bibi Zetu…” ndiyo baadhi ya maneno aliyoyatumia msanii huyo. Mwimbaji huyo ambaye awali alikuwa akiimba nyimbo za injili anasema hana ubaya wowote na wanamuziki wa Tanzania huku akitaja Diamond Platnumz na Alikiba ambao alisema ni marafiki wake.

Bahati anasema wakati umewadia kwa wanamuziki wa Kenya kuacha kufikiria kwamba kila mmoja anaweza kuafikia ufanisi kivyake na waungane.

Kulingana naye, Kenya ina wanamuziki bora, Kenya ndiyo inaongoza katika eneo la Afrika Mashariki hata kisiasa, mashindano ya kukimbia na hata uchumi na hivyo lazima irejeshe uongozi wake katika tasnia ya muziki katika kanda hii.

“Sina Ubaya, Sitafuti Kiki wala Chochote… Wengi wenu mnaufahamu moyo wangu, nia yangu ni kuona tukifika tunapostahili kuwa, juu kabisa.” alimalizia mwimbaji huyo.

Kulingana na picha ambazo alichapisha, nyimbo za wanamuziki wa Tanzania kama vile Diamond Platnumz, Alikiba, Marioo na Mbosso ndizo husikilizwa sana na wakenya zikifuatiwa na za wanamuziki wa Nigeria kama vile Kizz Daniel.

Mchekeshaji Eric Omondi amekuwa akiendeleza harakati za kutetea muziki wa Kenya humu nchini ambapo alikuwa anataka nyimbo zao zichezwe kwa wingi kwenye vyombo vya habari na wapatiwe kipaumbele na waandalizi wa matamasha.

Share This Article
Leave a Comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *