Bado hatujapokea hela, asema Gavana Barasa wa Kakamega

Martin Mwanje
2 Min Read

Gavana wa kaunti ya Kakamega Fernandes Barasa amekanusha madai ya kaunti zote 47 nchini kupokea fedha kutoka kwa serikali kuu. 

Barasa ametaja matamshi ya Waziri wa Fedha John Mbadi kuwa kaunti zimepokea fedha hizo kuwa ya kupotosha.

“Nataka kumwambia Waziri wetu wa National Treasury ya kwamba, Mheshimiwa John Mbadi, stop misleading Kenyans. Unajua ya kwamba pesa zikitoka katika National Treasury kwenda kwa County Revenue Fund ambayo inakuwa controlled by Central Bank, it takes a minimum of two weeks kwa hiyo pesa kufika katika magatuzi yote 47,” amesema Gavana Barasa.

“Because we have a lot of bureaucracy and inefficiency in the Office of the Controller of Budget.”

Gavana Barasa anasema fedha za mwezi Septemba zilitolewa na serikali kuu wiki jana na kwamba kufikia sasa, bdo hazijapokelewa na serikali za kaunti.

Kauli za Gavana huyo zinakuja wakati ambapo serikali kuu imesema kaunti zote 47 zimepokea mgao wake wa fedha unaopaswa kutolewa kufikia sasa.

Akiwajibu Magavana ambao awali walitishia kusimamisha shughuli za serikali za kaunti katika kipindi cha siku 30 zijazo kutokana na ukosefu wa fedha, Waziri Mbadi alisema jana Jumatatu kuwa jumla ya shilingi bilioni 158.024 zimetolewa kwa serikali za kaunti kufikia wakati huu.

Kulingana naye, Fedha hizo zinajumuisha deni la mwezi Juni pamoja na mgao wa fedha wa miezi ya Julai, Agosti, Septemba na Oktoba.

 

Share This Article