Mbunge wa Embakasi Mashariki katika kaunti ya Nairobi Babu Owino anahisi kwamba mpango wa lishe shuleni katika kaunti ya Nairobi, unafaa kusimamiwa na usimamizi wa kila shule na wala sio Gavana.
Kupitia akaunti zake za mitandao ya kijamii, Babu alitoa maoni kwamba kila shule iwe na jiko lililo na vifaa vyote hitajika pamoja na wapishi.
“Jikoni 10 za Gavana Sakaja haziwezi kulisha mamia ya wanafunzi katika kaunti ya Nairobi. Idadi ya jikoni ikilinganishwa na idadi ya wanafunzi ni ya kutiliwa shaka.” aliandika Babu.
Kiongozi huyo anadai kwamba chakula huwa kinacheleweshwa kila siku kwa sababu ya matatizo ya usafirishaji jambo ambalo huenda likatatiza ratiba za masomo katika taasisi hizo.
Alizua maswali kuhusu ada ambayo kila mzazi huhitajika kulipia mtoto kila siku ili apate chakula hicho ambayo ni shilingi tano kwa kila mwanafunzi ilhali kuna mgao wa lishe shuleni katika bajeti.
Mpango huo wa lishe shuleni kwa jina “Dishi na County” ulizinduliwa na Gavana Sakaja mgeni wa heshima akiwa Rais William Ruto.
Serikali ya kaunti ya Nairobi ilitenga shilingi Bilioni 1.7 kwa ajili ya mpango huo ambapo jikoni 10 za kisasa zilijengwa katika shule za msingi za Baba Dogo, Bidii, Kwa Njenga, Farasi Lane, Muthangari, Kayole One, Njiru, Toi, Roysambu na Racecourse.
Chakula hupikiwa humo na kusambazwa kwa shule nyingine ambazo zinanufaika na mpango huo.