Babake Nakaaya afariki

Marion Bosire
1 Min Read
Mzee Abraham Edward Sumari

Mwanamuziki wa asili ya Tanzania Nakaaya Sumari anaomboleza kifo cha babake mzazi ambacho kilitokea jana Jumapili Mei 12, 2024. Mzee Abraham Edward Sumari anaripotiwa kufariki akiwa jijini Dar es salaam.

Nakaaya alitangaza hayo kwenye akaunti yake ya Instagram ambapo aliandika ujumbe wa kumuaga babake. Aliandika, “Baba… Nitakupenda na kukuenzi milele, nakupenda sana… pumzika kwa amani simba wangu, pumzika kwa amani mfalme.”

Aliendelea kusema kwamba alijifunza jambo moja kutoka kwa marehemu babake ambalo ni ujasiri kwani alipenda sana kusema maneno “mimi siogopi” akiahidi kusalia mjasiri kama simba jike.

Mzee Sumari atazikwa nyumbani kwake katika kijiji cha Cairo, eneo la Mererani huko Arusha Jumatano Mei 15, 2024. Leo Jumatatu Mei 13, 2024 saa tano unusu asubuhi ibada ya kumuaga itaandaliwa katika hospitali ya Muhimbili.

Nakaaya alipata umaarufu baada ya kushiriki shindano la Afrika Mashariki la muziki lililofahamika kama Tusker Project Fame mwaka 2006 nchini Kenya na baada yake akarejea Tanzania akaanza kurekodi nyimbo.

Nakaaya Sumari

Albamu yake ya kwanza kwa jina “Nervous Conditions” ilizinduliwa Februari mwaka 2008.

Dadake mdogo ambaye anaitwa Nancy Sumari aliibuka mshindi wa shindano la urembo kwa jina Miss Tanzania mwaka 2005.

Share This Article