Siku chache baada ya waziri wa usalama wa taifa Prof. kithure Kindiki kutangazwa kuwa kiongozi wa kisiasa wa eneo la Mlima Kenya, migawanyiko ya kisiasa inaendelea kushuhudiwa katika eneo hilo, kuhusu ni nani kati yake na naibu Rais Rigathi Gachagua anapaswa kuwa kiongozi.
Kundi moja la wazee kutoka kaunti ya Embu, limejiotokeza kupinga vikali uteuzi wa Prof. kindiki kuwa kiongozi wa kisiasa wa eneo la Mlima Kenya.
Wazee hao wa baraza la Nyangi Ndiriri wakiongozwa na mwenyekiti wao Andrew Ireri, walikashifu hatua hiyo wakisema iliafikiwa na wazee wachche ili kuwgawanya kura za eneo hilo kabla ya uchaguzi mkuu wa mwaka 2027.
Akizungumza na wanahabari mjini Embu, Ireri aliwashutumu viongozi wanaovuruga siasa za eneo hilo kwa kumuidhinisha Prof. kindiki badala ya kukabiliana na maswala yanayoathiri kaunti hiyo.
“Wanazunguka na pesa wakiwahonga viongozi wengine kumuidhinisha Kindiki, lakini hakuna maendeleo wamewafanyia wananchi,” alisema Ireri.
Ireri alitoa wito kwa Kindiki kukataa uteuzi huo na kuangazia uongozi bora badala ya kuingia katika propaganda za uchaguzi wa mwaka 2027.
Awali viongozi waliochaguliwa walimuidhinisha Kindiki kuwa kiongozi wa eneo hilo, hatua iliyoungwa mkono na wazee wa Njuri Ncheke waliojitenga na mremgo wa naibu Rais Rigathi Gachagua.