Huku sehemu nyingi za nchi zikiendelea kushuhudia msimu wa mvua, maeneo mbalimbali Jijini Nairobi na Machakos yamearithiwa pakubwa na mafuriko na kuwaacha watu wengi bila makao.
Kulingana na shirika la msalaba mwekundu hapa nchini, mitaa ya Fuata Nyayo, Kibra, Mukuru Kwa Njenga, Kayole Soweto, Lavington, na Kawangware, imeathiriwa, na kusababisha shirika hilo kubuni makundi ya kuokoa yanayojumuisha maafisa kutoka shirika hilo na serikali za kaunti husika.
Katika kaunti ya Machakos, mto Athi ulivunja kingo zake na kusababisha watu 19 kukwama katika eneo la Kinanie. Hata hivyo watu 14 kati yao waliojumuishwa watu wazima 10 na watoto 4 waliokolewa, huu juhudi za kuwaokoa waliosalia zikiendelea.
Gavana wa kaunti ya Machakos Wavinya Ndeti ametoa wito wa juhudi za dharura, kufuatia mafuriko katika maeneo ya Kinanie na Syokimau.
Idara ya utabiri wa hali ya hewa, iawali ilitoa tahadhari kuwa baadhi ya maeneo hapa nchini yatakabiliwa na changamoto kutokana na mafuriko.