Halmashauri ya Ustawishaji Majani Chai Nchini, KTDA, imeagiza tani 92,737 za mbolea itakayouzwa kwa wakulima wa mashamba madogo ya majani chai.
Mbolea hiyo aina ya NPK, ilinunuliwa moja kwa moja kutoka Urusi.
Meli ya kwanza iliyosafirisha mbolea hiyo iliwasili katika bandari ya Mombasa jana Jumatatu ikiwa na tani 47,800 za mbolea hiyo (magunia 956,0000 ya kilo hamsini kila moja), huku meli ya pili ikitarajiwa kuwasili mwezi Novemba.
Bei ya mbolea imeathiriwa na ongezeko la bei ya gesi ambayo ni muhimu katika utengenezaji wa mbolea hiyo ya NPK, viwango vya juu vya kubadilisha sarafu za kigeni, bei za juu za mafuta ghafi na gharama za usafirishaji miongoni mwa masuala mengine.
Bei ya mfuko mmoja wa kilo hamsini ya mbolea hiyo itaafikiwa, baada ya kushughulikiwa kwa bei ya usafiri hadi viwanda vya majani chai na bima ya majani hayo.
KTDA hununua mbolea kwa ajili ya wakulima 650,000 wa mashamba madogo, ambao ni wadau katika viwanda vinavyosimamiwa na halmashauri hiyo, kupitia mfumo wa zabuni wa Kimataifa ulio na ushindani.
Mbolea hiyo kisha husambazwa kwa wakulima hao kupitia viwanda vyao vya majani chai.
Mpango huo huwawezesha wakulima wadogo wa majani chai kupata mbolea ya ubora wa hali ya juu kwa bei nafuu.