AU yatoa wito wa kutatuliwa kikamilifu kwa chanzo kikuu cha mzozo wa DRC

Tom Mathinji
1 Min Read
Mwenyekiti wa Umoja wa Afrika Mahmoud Ali Youssouf.

Umoja wa Afrika umetoa wito kwa wadau kusuluhisha chanzo cha mzozo unaoghubika Jamhuri yaKidemokrasia ya Congo (DRC), ili kuhakikisha amani ya kudumu inapatikana.

Akizungumza wakati wa mkutano kati ya Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) na ile ya Kusini mwa Afrika (SADC), ulioongozwa kwa pamoja na wapatanishi wa mzozo wa DRC katika Ikulu ya Nairobi, Mwenyekiti wa Umoja wa Afrika (AU) Mahamoud Ali Youssouf, aliwahimiza viongozi kudhihirisha ujasiri na hekima katika kuleta amani katika kanda hiyo.

“Tunawahimiza wadau wote kushughulikia chanzo cha mzozo kwa njia iliyo bora zaidi. Ili kupatikana kwa amani ya kudumu lazima kuwe na  ujasiri, hekima na kujitolea. Tuna imani kwamba viongozi wa kanda hii wanauwezo wa kutekeleza haya,” alisema Youssouf.

Alithibitisha jukumu muhimu katika kutatua mizozo barani humu, akisema Baraza la Usalama na Amani la Umoja huo limejitolea katika juhudi hizo.

Mkutano huo ulioongozwa kwa pamoja na Rais William Ruto na mwenzake wa Zimbabwe Emmerson Mnangagwa, uliwaleta pamoja viongozi kutoka EAC, SADC,  AU kujadili mikakati ya kuleta udhabiti Mashaiki mwa DRC, eneo ambalo limekumbwa na utovu wa usalama kwa muda wa miongo kadhaa.

Website |  + posts
Share This Article