Athari za ukame: Wakazi wa North Horr, Marsabit bado wanahangaika

Kbc Digital
2 Min Read

Angalau asilimia 90 ya wakazi wa eneo bunge la North Horr, kaunti ya Marsabit bado wanahangaika kuzipiga dafrau athari za ukame ulioshuhudiwa katika eneo hilo kati ya mwaka 2019 na 2022.

Wakizungumza wakati wa zoezi la usambazaji chakula cha msaada uliofanywa na shirika lisilokuwa la kujipatia faida la Korea Kusini la Good Neighbors, wakazi walielezea changamoto ambazo familia kadhaa zimelazimika kukabiliana nazo kutokana na mabadiliko ya tabia nchi.

Abudho Tuye kutoka kijiji cha Korka, alisimulia inayoumiza kwa wazazi kuwaona wanao wakilala bila chakula kwa siku mbili hadi tatu pale msaada wa chakula unapokosekana kutoka kwa wahisani.

Tuye ni miongoni mwa wfugahi waliopoteza mifugo isiyopungua 300,000 katika kaunti ya Marsabit kutokana na ukame.

Ni matamshi yaliyoungwa mkono na mbunge wa North Horr Wario Adhe Guyo alielezea wasiwasi juu ya matatizo si haba wanayokumbana nayo wakazi wa eneo hilo. Alielezea kuhuzunika kwake kwamba wazazi kadhaa bado wanahangaika kuwapeleka wanao shuleni kutokana na ukosefu wa karo na lishe bora.

Aidha, mbunge huyo alilalamika kuwa familia zilizoathiriwa hazipati tena usaidizi licha ya kwamba bado zinakabiliwa na changamoto.

Namun Hea, Mkurugenzi wa shirika la Good Neighbours nchini Kenya ametoa wito kwa washirika wote kutoa kipaumbele kwa miradi ya muda mrefu itakayosaidia kukabiliana na athari za ukame katika eneo hilo.

Taarifa yake Bruno Mutunga 

Share This Article
Leave a Comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *