Chombo cha habari kinachomilikiwa na serikali nchini Urusi kimeripoti kwamba Rais aliyebanduliwa madarakani wa Syria Bashar al-Assad yuko jijini Moscow.
Assad amepatiwa hifadhi humo saa chache baada ya Wizara ya Mambo ya Nje ya Urusi kutangaza kwamba alijiuzulu na kuondoka Syria.
Wapiganaji wa upinzani nchini Syria nao walitangaza kukamilika kwa utawala wa Al-Assad wa miaka 24, baada yao kuuteka mji mkuu wa Damascus.
Amri ya kutotoka nje usiku imetangazwa jijini Damascus baada ya watu wengi kujitokeza kwenye barabara za jiji hilo na kwingineko kusherehekea kupinduliwa kwa serikali ya Al-Assad.
Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu naye ametangaza kwamba wanajeshi wa nchi yake wamechukua udhibiti wa eneo lisilokaliwa karibu na Golan Heights baada ya mapinduzi.
Israel imetekeleza mashambulizi kadhaa ya angani katika maeneo mbalimbali ya Syria, matukio yanayojiri baada ya wapiganaji wa upinzani nchini Syria kuteka miji kadhaa.
Waasi hao walifungulia wafungwa huku mmoja wa waliojipatia uhuru akielezea kwamba alipokuwa gerezani hakuwa na jina ila alitambuliwa tu kwa nambari.
“Nilikamatwa na serikali na familia yangu ilidhania kwamba nilishafariki. Hawakujua niliko. Wafungwa wenza pia walichukuliwa bila ufahamu wa familia zao,” alielezea mfungwa huyo.
Kundi jingine la wafungwa lilielezea kwamba uhuru wao ulijiri siku ambayo walikuwa wamepangiwa kuuawa.