Mhubiri Gilbert Deya ameondolewa mashtaka ya ulanguzi wa watoto kutokana na ukosefu wa ushahidi wa kutosha.
Hakimu Robinson Ondieki alisema kwamba Deya hakuhusika kwenye wizi wowote wa watoto kwani wakati kisa hicho kilichotendeka mwaka 2004, alikuwa nchini Uingereza. Aliongeza kuwa upande wa mashtaka haukutoa ushahidi wa kutosha wa kuambatanisha mshtakiwa na mashtaka.
Katika uamuzi wake, Hakimu alisema mkewe Gilbert Deya, Mary Deya, aliachiliwa huru na mahakama ya Kibera hata ingawa alikuwa ameshtakiwa kwa kosa hilo hilo.
Deya kupitia kwa wakili wake John Swaka aliiambia mahakama kwamba ni jukumu la upande wa mashtaka kutoa ushahidi wa kutosha hata baada ya kutumia pesa nyingi kumsafirisha Deya kutoka nchini Uingereza kufuatia agizo la mahakama la kumhamishia nchini Kenya ili ashtakiwe nchini.
Akizungumza nje ya mahakama muda mfupi baada ya kesi yake kutupiliwa mbali, Deya alisema sasa yuko huru na atarejelea kazi ambayo Mungu alimteua kutekeleza ulimwenguni. Alishukuru serikali ya Uingereza ambayo alisema ilimtunza kwa miaka 12. Alikumbuka pia kwamba yeye ndiye alianzisha mpango wa kuhubiri kwenye runinga ya KBC kisha akafuatiwa na Askofu Mark Kariuki.
Gilbert Deya wakati huo, alikuwa akihubiri kwamba alikuwa na uwezo wa kuwafanya kina mama wasio na uwezo wa kupata watoto waweze kupata watoto. Baadaye, ilisemekana kwamba watoto ambao walikuwa wakikabidhiwa waumini kama hao walikuwa wa kuibwa.