Nahodha wa zamani wa timu ya taifa ya Ghana Asamoah Gyan amesema anaangazia kufungua akademia ya kutoa mafunzo ya soka nchini mwao kama njia ya kukuza vipaji na kuinua viwango vya soka.
Gyan kwenye mahojiano ya kipekee na KBC jijini Rabat, amesema mchezo wa soka umebadilisha maisha yake pakubwa na angependa kuona chipukizi pia wakikua kimchezo.
Mshambulizi huyo aliye na umri wa miaka 37, alitangaza kustaafu kutoka soka Juni 23 mwaka huu baada ya kucheza kwa zaidi ya miongo miwili. Pia ana imani kuwa bara la Afrika lina uwezo wa kuandaa fainali za Kombe la Dunia kwa mara ya pili hususan katika ombi la pamoja la Morocco, Uhispania na Ureno kuandaa kipute hicho mwaka 2030.
Gyan ndiye mfungaji bora katika historia ya timu ya taifa ya Ghana kwa magoli 51 na pia anashikilia rekodi ya mchezaji wa Afrika aliyepachika mabao mengi zaidi katika fainali za Kombe la Dunia kwa magoli 6.