Anjella atangaza kwamba ameacha muziki wa dunia

Hatima ya ushirikiano uliotarajiwa kati ya Anjella na Zuchu haijulikani sasa.

Marion Bosire
2 Min Read
Anjella, Mwanamuziki wa Tanzania

Mwanamuziki wa Tanzania Anjella ametangaza kwamba ameacha muziki wa dunia. Kupitia Instagram, mwimbaji huyo aliiaga Bongo Fleva akisema hatairudia tena kwani anarejea kwa Mungu ishara kwamba huenda akaanza kuimba nyimbo za injili.

“Bye bye bongo fleva hatutaonana tena narudi madhabahuni pa Mungu.” ndiyo maneno aliyotumia mwanamuziki huyo ambaye aliwahi kusajiliwa na kampuni ya Harmonize iitwayo Konde Music Worldwide.

Kabla ya hapo, Anjela alimshukuru sana Mungu kwa uhai, kwa waliomuunga mkono na kwa ajili ya Zuhura Othman almaarufu Zuchu.

Anasema Zuchu amekuwa wa baraka kwake na kwa familia yake. Mwezi Agosti mwaka 2024, Zuchu alimpa Anjella zawadi ya gari na baadaye akaahidi kushirikiana naye katika muziki.

Sasa haijulikani itakuwaje baada ya Anjella kuashiria kwamba ameacha kuimba nyimbo za kidunia.

Anjella ambaye jina lake halisi ni Angelina Samson George, alichupa katika tasnia ya muziki nchini Tanzania baada ya kufahamika na Harmonize kupitia mitandao mwezi Februari mwaka 2021.

Hii ni baada ya Harmonize kuona video ya Anjella akiimba kando ya barabara na akavutiwa na talanta yake.

Alishirikishwa na Harmonize kwenye kibao ‘All Night’ na tangu wakati huo akawa anatoa nyimbo kama vile, ‘Blessing’ na ‘Nobody,.

Novemba 2022 Anjella aliondoka kwenye kampuni ya Konde Music na akawa ni kama anadidimia hadi tena wakati ambapo alionekana na Zuchu.

Share This Article
Leave a Comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *