Serikali ya Marekani imewawekea vikwazo maafisa watatu wa serikali ya Mali kwa kile ilichokitaja kuwa kusaidia kupanuka kwa kundi la mamuluki la Wagner kutoka Urusi katika eneo la Afrika magharibi.
Walioathirika na vikwazo hivyo ni Waziri wa Ulinzi Kanali Sadio Camara, Mkuu wa jeshi la anga Kanali Alou Boi Diarra na Naibu Mkuu wa wanajeshi Kanali Adama Bagayoko.
Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani Anthony Blinken alitoa taarifa kuhusu watatu hao jana Jumatatu ambapo aliwanyoshea kidole cha lawama kwa kusaidia kupanua uwepo wa kundi la Wagner nchini Mali tangu mwezi Disemba mwaka 2021.
Aliongeza kwamba vifo vya raia vimeongezeka maradufu tangu mamluki hao wa Urusi kuingia nchini humo. Vingi kati ya vifo hivyo, Blinken alisema, vilisababishwa na operesheni za wanajeshi wa Mali wakisaidiwa na kundi hilo.
Brian Nelson wa Wizara ya Fedha nchini Marekani kwenye taarifa tofauti, alisema maafisa hao wa Mali wamekuwa nguzo muhimu katika kuwezesha kundi la Wagner kuimarika nchini Mali katika muda wa miaka miwili sasa.
Aliongeza kuwa maafisa hao wamekuwa wakiweka watu wao katika mazingira magumu ya vitendo vya uharibifu vinavyotekelezwa na kundi la Wagner pamoja na ukiukaji wa haki zao kwa nia ya kutumia vibaya rasilimali za Mali kupendelea operesheni za kundi la Wagner nchini Ukraine.
Marekani na washirika wake wamekuwa wakitoa vikwazo kwa kundi la Wagner na washirika wake kwa miaka mingi sasa.
Wiki jana, Uingereza iliweka vikwazo dhidi ya watu 13 kutoka Jamhuri ya Afrika ya Kati, Mali na Sudan wanaohusishwa na kundi la Wagner.