Marekani yasitisha usaidizi wa kifedha kwa Niger

Marion Bosire
2 Min Read

Marekani imetangaza kusitishwa kwa misaada ya kifedha kwa taifa la Niger kufuatia mapinduzi. Haya yalisemwa na kaimu naibu waziri wa mambo ya nje nchini Marekani Victoria Nuland jijini Niamey nchini Niger.

Aliandaa mazungumzo na baadhi ya viongozi wa mapinduzi nchini Niger ambayo aliyataja kuwa wazi na magumu.

Marekani inaamini mgogoro wa nchi hiyo ya Afrika Magharibi unaweza kumalizwa kidiplomasia na Rais Mohamed Bazoum arudishwe madarakani lakini kwa sasa wamesitisha malipo ya misaada.

Huku haya yakijiri, nchi wanachama wa jumuiya ya kiuchumi ya Afrika Magharibi, ECOWAS wanapanga mkutano jijini Abuja nchini Nigeria Alhamisi kujadili tatizo la Niger.

ECOWAS ilikuwa imetoa makataa ya siku 15 kwa wanajeshi wa Niger kurejesha mamlaka kwa Bazoum, makataa ambayo yalikamilika juzi Jumapili bila mabadiliko yoyote.

Badala yake, viongozi wa mapinduzi waliamua kufunga anga ya nchi hiyo kwa muda usiojulikana kwa kuhofia uvamizi wa kijeshi kutoka nchi jirani.

Nuland alielezea kwamba kwenye kikao hicho na viongozi wa mapinduzi, alipitisha ujumbe kwamba Marekani ilikuwa tayari kuwasaidia iwapo walikuwa na nia ya kurejesha uongozi wa kikatiba.

Alisema hakuona kama kujitolea kwa Marekani kulipokelewa kwa vyovyote.

Alifafanua kwamba alikutana na mkuu mpya wa majeshi nchini Niger Brigadia jenerali Moussa Salaou Barmou na sio kiongozi wa kijeshi wa Niger jenerali Abdourahamane Tchiani au Rais Bazoum.

Share This Article
Leave a Comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *