Ambassadors of Christ kuadhimisha miaka 30

Hafla hiyo itaandaliwa Jumapili hii inayokuja katika ukumbi wa BK Arena, jijini Kigali.

Marion Bosire
1 Min Read

Kwaya ya Ambassadors of Christ ya Kanisa la Waadventista Wasabato, SDA kutoka Rwanda, Jumapili hii itaadhimisha miaka 30 ya huduma na muziki katika ukumbi wa BK Arena, jijini Kigali.

Sherehe hiyo ya Agosti 30, 2026, itawakutanisha waimbaji wa kwaya, wafuasi na wageni mbalimbali kwa ajili ya kuadhimisha miongo mitatu ya huduma na kutafakari safari ya kundi hilo.

Katika ujumbe aliouchapisha kwenye mitandao ya kijamii, Sarah Sanyu, mmoja wa waimbaji wa kwaya hiyo, alisema kundi hilo limekuwa halifanyi shughuli nyingi hivi karibuni kutokana na maandalizi ya sherehe hiyo kubwa.

“Kwa kweli Mungu amechora hadithi yetu tangu mwanzo hadi sasa,” alisema Sanyu, huku akiwaalika watu kuungana nao katika sherehe hiyo na kushuhudia wema na uaminifu wa Mungu.

Pia aliwashukuru wafuasi kwa uvumilivu, upendo na kuendelea kuwaunga mkono katika kipindi ambacho shughuli za kwaya zilipungua.

Kwa mujibu wa Sanyu, kwaya hiyo inatarajia kurejea ikiwa imara na yenye shughuli nyingi zaidi baada ya sherehe hizo.

Pia aliwaalika watu na mashirika yanayopenda kusaidia kuitangaza kazi ya kwaya hiyo na kuifikisha kwa watu wengi zaidi kuwasiliana nao.

Sherehe hiyo katika BK Arena inatarajiwa kuwa hatua muhimu katika historia na huduma ya kwaya hiyo.

Share This Article