Aliyekuwa msaidizi wa kinara wa Azimio Raila Odinga Silas Jakakimba amejiunga na chama cha United Democratic Alliance (UDA).
Jakakimba alichukua uamuzi huo jana Jumanne, miezi kadhaa baada ya kukihama chama cha Orange Democratic Movement (ODM).
Amefichua kuwa alijiondoa ODM ili kuunga mkono sera za utawala wa Rais William Ruto.
Akizungumza baada ya kupokelewa rasmi na Katibu Mkuu wa UDA Cleophas Malala, Jakakimba alisema kujiunga kwake kwa chama hicho ni dhihirisho la umaarufu wake nchini kote na eneo la Nyanza.
“Leo, niko hapa kutangaza kuingia kwangu rasmi katika chama cha United Democratic Alliance Party of Kenya,” alisema Jakakimba.
“Ninakusudia kujiunga na watu wengi wa Nyanza ambao sasa wanazidi kuwa tayari kuhamasisha, kutangaza na hata kugombea uchaguzi kwenye jukwaa la UDA. Kujiunga na UDA kunathibitisha imani yangu kwamba chama hiki ni chama cha kitaifa chenye eneo bunge la kitaifa na mustakabali mzuri zaidi katika njia ya kuweka msingi na kuimarisha mafanikio ya kidemokrasia katika azima yetu ya miaka mingi ya utawala bora katika Jamhuri ya Muungano.”
Jakakimba amefanya kazi na Raila tangu mwaka wa 2004 na aligura ODM mwezi Machi mwaka 2023. Aliwania wadhifa wa useneta katika Kaunti ya Homa Bay mwaka wa 2022 lakini hakufaulu.
Mwanasiasa huyo anaazimia kuwania ubunge wa eneo la Suba Kaskazini. Wadhifa huo kwa sasa unashikiliwa na Millie Odhiambo ambaye yuko katika muhula wake wa tatu.