Aliyekuwa Gavana wa Murangá Mwangi Wa Iria, anazuiliwa katika gereza la Industrial Area, baada ya kukanusha mashtaka ya ufisadi, utumizi mbaya wa mamlaka, ukinzani wa maslahi, kujipatia mali kinyume na sheria na ulanguzi wa fedha dhidi yake.
Kupitia kwa taarifa katika mtandao wa X, tume ya maadili na kukabiliana na ufisadi EACC ilisema hakimu Thomas Nzioki, alimuachilia huru Wa Iria kwa dhamana ya shilingi milioni 20 au alipe shilingi milioni 10 pesa taslimu, lakini hakuweza kupata fedha hizo.
Kulingana na tume hiyo, Mwangi wa Iria na mke wake walinufaika moja kwa moja na shilingi milioni 562 ambazo zililipwa na serikali ya kaunti ya Murang’a kwa kampuni ya Top Image Media Consultants Limited, ambayo wakurugenzi wake ni Jane Wanjiru Mbuthia na David Maina Njeri.
“Sehemu ya fedha hizo zilitumwa kwa wakfu wa Mwangi wa Iria, huku kiwango kigine cha fedha hizo kikitumika kulipa mkpo wa Wa Iria katika benki ya CFC Stanbic,“ ilisema taarifa ya EACC.
Wakati huo huo mke wa Wa Iria na ndugu yake ambao ni wakurugenzi wa kampuni ya Value View Limited, walinufaika na fedha ambazo zililipwa kwa kampuni ya Top Image Media Consultant, kupitia ununuzi wa ardhi Jijini Nairobi na Nyeri na nyumba mbili za kifahari Nanyuki.