Mwanamuziki wa Uganda Alien Skin ambaye jina lake halisi ni Patrick Mulwana anaripotiwa kukamatwa na maafisa wa polisi jana Jumatano kwa tuhuma za kushambulia wahudumu wa hospitali ya Nsambya.
Msemaji wa polisi Kituuma Rusoke ndiye alitangaza kukamatwa kwa msanii huyo na kosa alilotenda na kuahidi ktoa taarifa zaidi baadaye.
Kukamatwa kwake kulijiri saa chache baada ya naibu msemaji wa eneo la Kampala Metropolitan Luke Owoyesigyire,kutangaza kwamba wanachunguza kisa cha kile kinachoweza kuwa mauaji na ushambuliaji.
Alielezea kwamba daktari mmoja na walinzi wawili walishambuliwa Jumanne usiku na kundi la watu waliokuwa wakiongozwa na Alien Skin katika hospitali hiyo ya Nsambya.
Taarifa ya polisi inaelezea kwamba Joram Tumwesigye wa umri wa miaka 28, mkazi wa eneo la Makindye alipokelewa hospitalini humo akiwa na majeraha mabaya.
Jamaa huyo alikata roho yapata saa moja baada ya kufikishwa hospitalini na Alien Skin mmoja wa waliompeleka huko akapandwa na hasira huku akitaka hati za hospitali za Tumwesigye kutoka kwa daktari aliyemhudumia.
Alipokosa kutekelezewa matakwa yake, Alien Skin na wenzake walimshambulia daktari na walinzi wawili kabla ya kutoroka eneo la tukio.
Walioshambuliwa walitambuliwa kama daktari Zaidi Matovu na walinzi Anthony Muyanda na Alex Odongo.
Alien Skin na wenzake wanachunguzwa pia kwa kosa la uporaji.