Alex Okosi ateuliwa Mkurugenzi Mtendaji wa Google Barani Afrika

Marion Bosire
2 Min Read

Kampuni ya Google imetangaza uteuzi wa Alex Okosi raia wa Nigeria kuwa Mkurugenzi Mtendaji wake barani Afrika.

Kabla ya kuteuliwa kwa wadhifa huo mpya, Okosi amekuwa akihudumu kama Mkurugenzi Mtendaji wa jukwaa la video YouTube katika eneo la Ulaya, Mashariki ya Kati na Afrika ambayo ni masoko yanayoibuka.

Alex anaamini teknolojia ina uwezo wa kuinua pakubwa maisha ya watu wa bara Afrika na kwa sababu hiyo, ana furaha kutunukiwa jukumu la kuongoza Google kuafikia hilo.

Raia huyo wa Nigeria ana tajriba katika masuala ya vyombo vya habari, burudani na teknolojia. Awali, alihudumu kama naibu rais na mkurugenzi mtendaji wa kampuni iitwayo “Viacom International Media Networks Africa” na nyingine iitwayo “BET International”.

Akiwa YouTube, Okosi alitekeleza jukumu muhimu la kuhakikisha ukuaji wa jukwaa hilo barani Afrika, Mashariki ya kati na Uturuki.

Kwenye kampuni ya Google, anatarajiwa kuendeleza mipango ya kusaidia katika ukuaji wa biashara na chumi za bara Afrika na upanuzi wa upatikanaji na utoaji wa vyombo vya kusaidia watumizi wapya kupata mengi kutoka kwenye mtandao huo.

Naibu Rais wa Google katika eneo la Ulaya, Mashariki ya kati na Afrika Meir Brand alimsifia Alex Okosi akimtaja kuwa kiongozi ambaye anapenda teknolojia na hivyo anaamini atatekeleza wajibu wake ipasavyo.

Kampuni ya Google imekuwa ikitekeleza kazi zake barani Africa kwa zaidi ya miaka 10 na ina afisi nchini Ghana, Kenya, Nigeria na Afrika Kusini. Bidhaa na huduma zake hutumiwa na wengi barani humu kila siku.

Share This Article