Afya kwa wote: Serikali kufanya kazi na sekta ya kibinafsi

Martin Mwanje
2 Min Read
Rais William Ruto amesema serikali itafanya kazi na sekta ya kibinafsi kuhakikisha upatikanaji wa afya kwa wote.
Amesema serikali itaunga mkono sekta ya dawa kuimarisha uwezo wake wa utengenezaji dawa humu nchini.
Aliongeza kuwa serikali itapitia upya mfumo wa kodi na gharama ya kufanya biashara katika sekta hiyo.
Kulingana na Rais Ruto, serikali itatoa kipaumbele kwa ununuaji wa bidhaa tiba kutoka kampuni zinazotengeneza bidhaa hizo humu nchini ili kukuza ukuaji wake.
“Utengenezaji wa bidhaa tiba humu nchini ni muhimu kwa upatikanaji wa afya kwa wote; upunguzaji wa gharama ya dawa na vifaa tiba utaifanya kuwa endelevu, ya bei nafuu na kufanya iwe mwafaka kwa kila mtu,” alisema Rais Ruto.
Aliyasema hayo leo Jumatano katika eneo la Syokimau, kaunti ya Machakos, wakati wa ufunguzi wa maaabara ya mikrobiolojia ya MEDS.
Maabara hiyo ya kisasa itatoa huduma za afya nchini Kenya na kanda hii.
Rais Ruto alidokeza kuwa serikali imetenga ekari 100 kati ya ekari 500 katika Ukanda Maalum wa Kiuchumi mjini Thika kwa ajili ya kampuni za utengenezaji dawa.
“Nawaalika wawekezaji kutumia nafasi hii kujenga viwanda vya utengenezaji dawa nchini Kenya,” alisema kiongozi wa nchi.
Aliongeza kuwa janga la virusi vvya korona lilizigutusha nchi kuhusiana na haja ya kuimarisha uwezo wao wa utengenezaji dawa.
Kwa upande wake, Waziri wa Afya Susan Nakhumicha alisema maabara hiyo ya MEDS ni maabara ambayo imetambuliwa na Shirika la Afya Duniani, WHO.
Alisema itapiga jeki utengenezaji dawa humu nchini na pia kuinua hadhi ya nchi katika sekta hiyo.
Share This Article