Mamlaka ya Udhibiti wa Nishati na Petroli nchini, EPRA imetangaza kupunguzwa kwa bei ya mafuta katika kipindi cha mwezi moja ujao kinachoanzia Juni 15-Julai, 14, 2024.
Kulingana na EPRA, bei ya mafuta ya petroli imepungua kwa shilingi 3, ile ya dizeli shilingi 6.08 na mafuta taa shilingi 5.71.
Mkurugenzi Mkuu wa mamlaka hiyo Daniel Kiptoo katika taarifa anasema kupungua huko kunatokana na kupungua kwa bei ya uagizaji wa bidhaa hiyo nchini.
Kutokana na mabadiliko hayo, lita moja ya petroli jijini Nairobi sasa itauzwa kwa shilingi 189.84, dizeli kwa shilingi 173.10 kwa lita na mafuta taa shilingi 163.05 kwa lita.
Jijini Mombasa, lita moja ya petroli itauzwa kwa shilingi 186.66, dizeli shilingi 169.93 kwa lita huku lita moja ya mafuta taa ikigharimu shilingi 160.00.
Jijini Nakuru, lita moja ya petroli itauzwa kwa shilingi 188.90, dizeli shilingi 172.54 kwa lita na mafuta taa kwa shilingi 162.57 kwa lita.
Mjini Eldoret, lita moja ya petroli itauzwa kwa shilingi 189.67, dizeli shilingi 173.31 kwa lita ilhali mafuta taa yatauzwa kwa shilingi 163.34 kwa lita.