Afueni kwa Seneta Orwoba, marufuku yapunguzwa hadi siku 30

Martin Mwanje
2 Min Read
Gloria Orwoba - Seneta mteule

Seneta mteule Gloria Orwoba ana kila sababu ya kutabasamu baada ya Bunge la Seneti kupunguza marufuku dhidi yake hadi siku 30. 

Hoja ya kupunguza marufuku hiyo iliwasilishwa leo Alhamisi na kiongozi wa wengi ambaye pia ni Seneta wa Kericho Aaron Cheruiyot.

Kisha hoja hiyo iliungwa mkono na kiongozi wa walio wachache  katika Bunge la Seneti ambaye pia ni Seneta wa Kilifi Stewart Madzayo.

Katika kuwasilisha hoja hiyo, Seneta Cheruiyot aliielezea kuwa Seneta  huyo tayari ameonyesha hali ya kujutia mienendo yake na kuomba msamaha, na kwamba kwa misingi hiyo, haitakuwa bora kukaa nje kwa muda mrefu.

Marufuku dhidi ya Seneta Orwoba ilianza kutekelezwa Februari 12 mwaka huu.

Wakati huo, tangazo la Seneta Orwoba kuanza kutumikia marufuku hiyo ya takriban miezi mitatu lilitolewa na Naibu Spika Kathuri Murungi.

Bunge la Seneti mwezi Septemba mwaka jana  kwa kauli moja lilipitisha hoja ya kumfungia nje Seneta huyo kwa ukaidi.

Hii ni baada ya Orwoba kutoa madai ya ufisadi na dhuluma za kunyanyaswa kimapenzi dhidi ya Maseneta wenzake.

Alipotakiwa kuyathibitisha, alishindwa kufanya hivyo na pia akadinda kufika mbele ya kamati ya nidhamu ya bunge hilo ili kujitetea.

“Naomba msamaha kwa bunge hili na yeyote ambaye nilimkosea katika kuwasilisha hoja yangu. Sikukusudia,” alisema Orwoba kabla ya kufunganya virago na kuondoka katika ukumbi wa Bunge la Seneti Februari 12 mwaka huu.

Seneta Orwoba alielekea mahakamani kupinga marufuku dhidi yake, kesi ambayo ilitupiliwa mbali na mahakama kukubaliana na uamuzi wa Seneti.

Alitarajiwa kutumikia marufuku hiyo hadi Mei 1, 2025.

 

Website |  + posts
Share This Article