Ni afueni kwa naibu Inspekta Jenerali wa polisi Gilbert Masengeli, baada ya Mahakama Kuu leo Ijumaa kuondoa kesi ya kuidharau mahakama iliyokuwa ikimkabili.
Mahakama hiyo ilikuwa imemhukumu Masengeli kifungo cha miezi sita gerezani, kwa kukaidi maagizo ya kufika mbele yake kuelezea waliko watatu watatu waliodaiwa kutekwa nyara katika mtaa wa kitengelea kaunti ya Machakos.
Huku akimwondolea Masengeli makosa hayo, Jaji wa Mahakama Kuu Lawrence Mugambi, alisema ameridhika na hatua ya naibu huyo Inspekta wa Polisi ya kuomba msamaha, na kwamba haikuwa hatua ya kumwadhibu ila kudumisha hadhi ya mahakama.
Ili kujiondoa lawamani, Masengeli kupitia hati ya kiapo, Masengeli alisema alikuwa akishughulikia masuala ya usalama wa kitaifa katika maeneo ya Pwani na Kaskazini mashariki mwa nchi.
Wakati huo huo Jaji Mugambi alijiondoa kusikiza kesi hiyo na kukabidhi suala hilo kwa Jaji Mkuu ili abuni jopo la kusikiza kesi hiyo kufuatia ombi jipya lililowasilishwa na chama cha mawakili hapa nchini-LSK.
LSK imewasilisha kesi kwa niaba ya wanaharakati Bob Njagi na kaka wawili ambao ni Jamil Longton na Aslam Longton, ambao yadaiwa walitekwa nyara mwezi uliopita katika kaunti ya Machakos. Watatu hao walipatikana leo asubuhi wakiwa hai katika kaunti ya Kiambu.