Kenya imepiga hatua kubwa baada ya Mamlaka ya Kusambaza Dawa Nchini (KEMSA) kutia saini makubaliano ya kutibu aina mbalimbali za ugonjwa wa saratani nchini ambao umeibuka kuwa tishio kwa maisha ya wengi.
Rais William Ruto alikuwapo wakati mamlaka hiyo ilipotia saini makubaliano hayo na kampuni ya dawa na bioteknolojia ya Marekani ya Pfizer.
Hafla ya utiaji saini makubaliano hayo ilifanyika katika Ikulu ya Nairobi na kuhudhuriwa na Mwenuekiti na Afisa Mkuu Mtendaji wa kampuni ya Pfizer Albert Bourla na Waziri wa Afya Aden Duale miongoni mwa maafisa wengine.
“Kutokana na hilo, bei za dawa ya kutibu saratani za matiti, tumbo, utumbo mpana, mapafu, tezi dume, umio, damu, tezi za limfu na saratani ya uboho zimepungua kwa kiwango kikubwa kwa zaidi ya mara 7,” alisema Ruto wakati wa hafla hiyo.
“Katika hali zingine, gharama imepungua kutoka shilingi za Kenya milioni 1 hadi chini ya shilingi 50,000 kwa kila mzunguko.”
Rais Ruto anasema makubaliano hayo yenye kichwa “Makubaliano kwa ajili ya Dunia yenye Afya” yatafanya shilingi 800,000 za kutibu saratani zilizotengwa na Mamlaka ya Afya ya Jamii (SHA) kutosheleza hata bila gharama za ziada kwa wagonjwa.
Chini ya makubaliano hayo, Kenya itapata dawa mpya bila wagonjwa wa saratani kusubiri kwa kipindi cha miaka 10 kama ilivyo kwa sasa.